Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’.
Andrew Carlos na Musa Mateja
OKTOBA 25, mwaka huu
ilikuwa ni moja kati ya siku za kihistoria nchini kwa Watanzania wote
kujumuika na kupiga kura za kuwachagua wabunge, madiwani na rais.
Siku hiyohiyo pia katika
Jiji la Milan, Italia kulikuwa na tukio la kihistoria kwa staa wa muziki
wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye alikuwa akiiwakilisha
Tanzania na Afrika kwa ujumla katika Tuzo za MTV Europe Music (EMA) na
kufanikiwa kuibuka na ushindi kupitia kipengele cha Best Worldwide Act:
Africa/India ambacho alikuwa akichuana na mwanamuziki maarufu wa India,
Priyanka Chopra aliyewahi kuwa pia Miss World mwaka 2000.
Uso kwa uso na mastaa ulaya
Kati ya matukio ambayo
Diamond anasema hawezi kuyasahau ni pamoja na kupata shavu la kukutana
na mastaa kibao wa ulaya ambao walipafomu na wengine kuchukuwa tuzo.
“Nimekutana na mastaa wengi
ambao sikuwahi kukutana nao kabisa zaidi ya kuwaona tu kwenye mitandao
na TV. Mastaa hao ni pamoja na Jason Deluro ambaye pia alipafomu Wimbo
wa Want to Want, Pharrel Williams naye alipafomu Wimbo wa
Freedom.“Nilipata bahati pia ya kuwashuhudia mastaa wengine kama vile
Justin Bieber, Ed Sheeran na wengine kibao,” alisema Diamond.
Bieber anyakua 5 kwa mpigo
Staa wa Pop, Justin Bieber aliweka historia kwake katika tuzo hizo baada ya kuibuka na tuzo tano kwa mpigo.
Staa huyo aliyepanda
jukwaani na kupiga ngoma yake mpya ya What Do You Mean alifanikiwa
kuibuka na tuzo katika vipengele vya Best Male, Best Look, Worldwide
Act: North America, Biggest Fans na Best Collaboration.
Mastaa wengine waliochukua
tuzo hizo ni Nicki Minaj, One Direction, Macklemore, Taylor Swift, Ed
Sheeran, Rihanna na wengine kibao.
Wazungu wapagawa na Diamond
Katika hali ya kushangaza
mapema kabla ya kuanza kwa sherehe hizo za utoaji tuzo, Diamond
aliyekuwa amevalia suti nyeupe alitinga ‘red carpet’ na kushangaa
kuvamiwa na wazungu waliookuwa wamepanga foleni kuwasubiri mastaa huku
kila mmoja akiwa na simu yake mkononi akitaka kupiga picha naye
(selfie).
Washindi waliopita
Katika kipengele
alichoshinda Diamond, alitanguliwa na Abdelfattah Grini (Morocco)
aliyechukuwa mwaka 2011, Ahmed Soultan (Morocco) mwaka 2012 na 2013 na
wa mwisho alikuwa Mohamed Assaf (Palestina).
Diamond anasemaje?
Kutokana na ushindi huo
uliokuja Tanzania na Afrika kwa ujumla, Diamond alifunguka mengi ya
kushukuru kwa wale wote waliompigia kura na kuahidi kufanya makubwa
zaidi ya hayo katika kazi zake za muziki.
“Nimeshangazwa sana kwa
namna ambayo nimepokelewa kwa kishindo nchini Italia. Wazungu
wamenionesha thamani ya juu kwa mapokezi makubwa na kunishangilia na
kunipongeza kwa tuzo niliyoipata. Nasema asanteni sana Watanzania
wenzangu kwa sapoti mlionionesha mwanzo mwisho hadi kwa kunipigia kura
na kufanikiwa kuibuka mshindi kutoka Afrika,” alisema Diamond.
Diamond alifanikiwa kupita
tano bora Afrika katika Tuzo za Ema baada ya kupigiwa kura za kutosha na
mashabiki wake kupitia mtandao wa Twitter. Wasanii wa Afrika aliokuwa
akichuana nao kabla ya kutua Italia ni Yemi Alade (Nigeria), Davido
(Nigeria), AKA (Afrika Kusini) pamoja na Wizkid (Nigeria).
No comments:
Post a Comment